SHINA LA UHAI: Upangaji Uzazi Umeongezeka, Lakini Elimu Bado Haijakolea

NA LEONARD ONYANGO

 

JOSEPHINE Atieno alipoenda katika kituo cha afya kusaka ushauri kuhusu mbinu mwafaka ya kumsaidia kuzuia ujauzito kwa muda mrefu, madaktari walimwambia kuwa kifaa kinachotiwa katika ngozi ya mkono (contraceptive implants) kingemfaa zaidi.

Kifaa hicho ambacho hutoa homoni za kuzuia mbegu za kiume kuingia kwenye yai, huwekewa wanawake wanaotaka kufunga uzazi kwa muda mrefu.

“Nilihofia kwamba huenda ningepata ujauzito mwingine kabla ya mtoto wangu wa kwanza kutambaa. Hivyo niliamua kwenda hospitalini kufunga uzazi kwa muda,” anasema Bi Josephine, ambaye ni mkazi wa Bondo, Kaunti ya Siaya.

Lakini anasema kuwa daktari hakumwelezea matatizo mengine ya kiafya yanayosababishwa na kifaa hicho baada ya kuwekwa mwilini.

Baadhi ya madhara aliyopata ni hedhi ambayo ilidumu kwa wiki mbili, chunusi zilizagaa usoni, maumivu ya kichwa, uchungu kwenye matiti, kichefuchefu, unene kupindukia, kizunguzungu na kubadilika hisia.

“Kuna wakati sikutaka hata kumwona mume wangu. Hisia zangu zilikuwa zikibadilika kila mara na sikuelewa shida yangu ni gani. Wakati mwingine sikuwa na hisia za kushiriki mapenzi na mume wangu,” anaelezea.

Kabla ya kuwekewa kifaa hicho mkononi, Bi Josephine anasema kuwa alikuwa na uzani wa kilo 54.

“Baada ya miaka miwili, nilianza kuongeza uzani hadi nikafikisha kilo 87. Wakati mwingine nilikuwa nashindwa kutembea,” anasema.

Naye Bi Angeline Ng’etich ameanza kuingiwa na wasiwasi kwamba sindano aliyodungwa kuzuia ujauzito kwa mwaka mmoja ndiyo imemzuia kupata mimba ya mtoto wa pili miaka miwili baadaye.

Anashutumu mhudumu wa afya aliyemdunga sindano hiyo kwa “kutoniambia ukweli kuhusu athari za ya sindano hiyo”.

“Natamani kupata mtoto wa pili lakini nimeshindwa kupata ujauzito. Tangu niache kuitumia miezi kumi liyopita, sijapata hedhi. Sitawahi kupanga uzazi tena,” akasema Bi Ng’etich.

Utafiti uliofanywa na shirika la Performance Monitoring For Action (PMA) kwa ushirikiano na wizara ya Afya katika kaunti 11 nchini umefichua kuwa karibu nusu ya akina mama wanaoenda katika vituo vya afya kusaka huduma za kupanga uzazi, hawaelimishwi kuhusu athari za pembeni za sindano, tembe au vifaa wanavyowekewa.

Utafiti huo ulifanywa katika Kaunti za Pokot Magharibi, Bungoma, Kakamega, Siaya, Nandi, Kericho, Nyamira, Kiambu, Nairobi, Kitui na Kilifi ambapo ilibainika kuwa asilimia 43 ya akina mama wanaosaidiwa kupanga uzazi hawapewi elimu kuhusu matatizo yanayotokana na mbinu hizo za kuzuia mimba.

Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya akina mama wanaotumia njia za kiasili kupanga uzazi imeongezeka nchini.

Miongoni mwa njia za kiasili zinazotumiwa kupanga uzazi ni matumizi ya kujiepusha kushiriki mapenzi katika ‘siku hatari’ – siku ambazo yai la mama huwa tayari kupokea mbegu za kiume.

Bi Mildred Waithera anasema kuwa aliamua kutumia njia za kiasili baada ya kukosa vifaa alivyokuwa akitumia kupanga uzazi katika hospitali za umma.

“Nilikuwa natumia kifaa kinachoingizwa ukeni kinachofahamika kama ‘copper coil’. Nilipendelea kutumia kifaa hicho kwa sababu kilikuwa hakinisababishii matatizo ya kiafya kama vile kunenepa au kuumwa na kichwa. Nilipoenda katika hospitali mbalimbali bila kukipata, niliamua kukumbatia mbinu za kiasili,” anasema Bi Waithera.

Takwimu za wizara ya Afya zinaonyesha kuwa nyingi ya hospitali za umma zilikuwa zimesalia na aina tatu pekee za dawa za kupanga uzazi kufikia Novemba 2021.

Hiyo inamaanisha kuwa akina mama waliokuwa wakitumia mbinu nyingine za kisasa walikosa huduma hizo au walilazimika kwenda katika hospitali za kibinfasi ambapo wanatumia fedha nyingi.

Kulingana na PMA, hospitali za umma huishiwa mara kwa mara dawa hizo kutokana na kuongezeka kwa idadi ya akina mama ambao wamekumbatia upangaji wa uzazi.

Ripoti ya Hali ya Uchumi nchini iliyoandaliwa na Shirika la Takwimu (KNBS), inaonyesha kuwa idadi ya akina mama wanaotumia mbinu za kisasa za kupanga uzazi ilipingua mwaka 2021 ikilinganishwa na 2020.

Prof Peter Gichangi, mtafiti mkuu wa PMA Kenya anasema kuwa japo mbinu za kiasili za kupanga uzazi ni salama – hazina matatizo ya kiafya. Lakini uwezo wa mbinu hizo za kiasili kuzuia mimba ni mdogo ikilinganishwa na mbinu za kisasa.

“Wanawake wanaweza kutotumia mbinu za kisasa za kupanga uzazi kutokana na imani za kidini au wanaogopa matatizo mengine ya kiafya yanayosababishwa na mbinu hizo. Lakini ukweli ni kwamba uwezo wa mbinu za kiasili kuzuia mimba ni mfinyu mno ikilinganishwa na hospitalini,” anasema Dkt Gichangi.

Kituo cha Kukabili Maradhi (CDC) kinasema kuwa wanawake wawili kati ya 10 wanaotumia mbinu za kiasili kupanga uzazi hujipata na mimba.

Ripoti ya PMA inasema kuwa japo idadi kubwa ya wanawake walioolewa wanatumia njia za kupanga uzazi, idadi kubwa ya vijana wa kike wanaotumia mbinu za kukinga ujauzito iko chini.

Asilimia 60 ya vijana hao hawatumii mbinu za kuzuia mimba, kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Kenya inalenga kuhakikisha kuwa idadi ya akina mama wanaotumia mbinu za kisasa kupanga uzazi inaongezeka kutoka asilimia 58 hadi 64 kufikia 2030.

Lakini Dkt Dan Okore wa Hazina ya Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Idadi ya Watu (UNPF) anasema kuwa huenda lengo hilo lisiafikiwe iwapo serikali haitachukua hatua za haraka kukabili changamoto zinazosababisha akina mama kukumbatia mbinu za kiasili na kuacha mbinu za kisasa.

Source: https://taifaleo.nation.co.ke/shina-la-uhai-upangaji-uzazi-umeongezeka-lakini-elimu-bado-haijakolea/